Tuesday 23 April 2024

TAKUKURU RAFIKI YASAIDIA KUTATUA KERO ZA ARDHI SHINYANGA.. MLEPA, NDALA WAPEWA NAMBA ZA VIWANJA

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy akizungumza na waandishi wa habari


Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog

Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Shinyanga (TAKUKURU) kupitia Program ya TAKUKURU RAFIKI imesaidia kutatua kero za wananchi mkoani Shinyanga.

Akitoa akitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi za TAKUKURU kwa kipindi cha robo ya tatu ya Januari hadi Machi 2024 leo Jumanne Aprili 23,2024 Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy amesema Programu ya TAKUKURU imefanya ufuatiliaji wa majibu ya kero ya kutopimwa maeneo ya makazi kwa wananchi wa kata ya Ndala Mtaa wa Ndala tangu mwaka 2018.


“Awali wananchi zaidi ya 246 walichanga kiasi cha shilingi 12,396,000/= na kulipa Manispaa ya Shinyanga kwa ajili ya zoezi la upimaji ardhi. Pia wananchi 1150 wa mtaa wa Mlepa waliokuwa wamechanga fedha kwa ajili ya kupimiwa na kurasimishiwa maeneo yao lakini walikuwa bado hawajapatiwa namba za upimaji wa viwanja vyao tangu mwaka 2023 walipopimiwa”,amesema Kessy.


“Wananchi wa mtaa wa Ndala walitoa keto yao kutopimiwa na kurasimishiwa maeneo yao pamoja na kuwa walikwishachangia huduma hiyo tangu mwaka 2018. Vilevile wananchi wa mtaa wa Mlepa kero yao ilikuwa kupatiwa namba za viwanja vyao tangu walipopimiwa mwaka 2023”,ameeleza.

Amesema hali hiyo ilikuwa inapelekea migogoro ya mipaka, kuwanyima fursa ya kupata mikopo katika taasisi za kifedha kwa kutumia ardhi kama dhamana lakini pia viwanja kutoongezeka thamani kwa kukosa utambuzi rasmi.


“Baada ya kupokea kero hiyo, TAKUKURU iliwasilisha Manispaa ya Shinyanga bango kitita lenye kero kusika na mikakati ya utatuzi wa kero hiyo. Halmashauri ya Manispaa Idara ya ardhi walishughulikia kero hiyo ambapo katika mtaa wa Mlepa zoezi la kugawa namba za viwanja lilianza na hadi sasa namba za viwanja 412 zimeanza kugawiwa tangu mwezi Januari na zoezi bado linaendelea”,amefafanua Kessy.

“Mwezi Februari Manispaa ya Shinyanga ilifanya zoezi la upimaji katika mtaa wa Ndala na kwa sasa Manispaa ipo kwenye mchakato wa ukamilishaji wa utengenezaji wa ramani kwa ajili ya kusajiriwa Wizarani na baada ya hapo kupata namba za viwanja hivyo 246 vya wananchi wa mtaa wa Ndala”,ameongeza.


Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga amesema TAKUKURU inaendelea kufuatilia ugawaji wa namba za viwanja vilivyopimwa katika mtaa wa Mlepa mpaka litakapokamilika lakini pia kufuatilia zoezi la ukamilishaji wa uandaaji wa namba za viwanja za mtaa wa Ndala na ugawaji wake.

Hali kadhalika TAKUKURU inaendelea kufanya vikao vya utambuzi wa kero katika kata 14 kutoka kata za Mwenge, Mwawaza, Kolandoto, Lyabukande, Puni, Nyida, Mhongoloi, Majengo, Nyasubi, Ulowa, Bulungwa, Mpunze, Bupigi na Bubiki.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy akizungumza na waandishi wa habari

Share:

MBOWE AONGOZA MAANDAMANO YA AMANI BUKOBA..ASISITIZA MAANDAMANO YANAENDELEA

Na Mbuke Shilagi Bukoba.

Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA wamefanya maandamano ya amani Aprili 22,2024 katika Mkoa wa Kagera wilaya ya Bukoba ambapo katika Kanda ya ziwa Victoria maandamano yameanzia Mkoa wa Kagera wilaya ya Bukoba na kuongozwa na mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Taifa Mh. Freeman Mbowe.

Maandamano hayo yamefanyika kwa kutembea na miguu kuanzia kata ya kashai ndani ya mtaa wa Mafumbo wakiwa na mwenyekiti wa CHADEMA Taifa akiwa pamoja na viongozi mbalimbali ngazi ya Kanda ya ziwa Victoria pamoja na viongozi wa Mkoa, Wilaya Kata Mitaa pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali mpaka uwanja wa Mayunga katika kata ya Bilele ambapo waliweza kuweka mkutano na kuzungumza na wananchi wa Kagera.

Aidha maandamano hayo yalikuwa ni kutaka kurekebishwa kwa mambo mbalimbali ndani ya serikali ambapo mabango yaliyobebwa na wananchi yalikuwa yameandikwa "Mfumuko wa bei za vyakula twafa" "bila haki hakuna amani" "Tunataka katiba mpya na tume ya uhuru ya uchaguzi" pamoja na mabango mengine mengi ambayo yalikuwa yanataka kupewa haki ambazo wamedhulumiwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA Taifa Mh. Freeman Mbowe amesema hakuna jambo linaloweza kuongeza hisia na mtazamo zaidi ya maandamano na kwamba maandamano siyo jambo la mzaha kwa sababu sio kila chama Cha siasa kinaweza kufanya maandamano maana maandamano ni ushawishi na ni turufu ya Chadema.

Pia amelipongeza jeshi la polisi Mkoa wa Kagera kwa kutoa ushirikiano kwa kuhakikisha kwamba maandamano yanakuwa yenye amani lakini pia kwa kuwa nao pamoja kwa ajili ya kulinda amani bega kwa bega.

Amesemavmaandamano hayo yataendelea ndani ya Kanda ya Ziwa Viktoria katika wilaya nyingine pamoja na Taifa kwa ujumla mpaka pale serikali itakapofanyia kazi kwa yote yanayotakiwa.

Amewashukuru wananchi kwa kujitokeza kupeleka ujumbe wa sauti zisizosikika ziweze kufika.

"Maandamano ni ujasiri na maandamano ni ukakamavu" ,amesema Mbowe.
Share:

Monday 22 April 2024

HAYA HAPA MAGAZETI YA LEO JUMANNE APRILI 23, 2024

           
Share:

DCEA YAKAMATA KILO 767.2 ZA DAWA ZA KULEVYA KATIKA OPERESHENI MAALUM, 21 MBARONI

KAMISHNA JENERALI wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za kulevya Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam
***


Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanya operesheni na kufanikiwa kukamata jumla ya kilo 767.2 za dawa za kulevya katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Tanga katika kipindi cha wiki mbili kuanzia Aprili 4 hadi 18, 2024.


Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, ametangaza mafanikio hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 22 Aprili, 2024, jijini Dar es Salaam na kusema kuwa, aina ya dawa zilizokamatwa ni pamoja na heroin (kilo 233.2), methamphetamini (kilo 525.67) na skanka (kilo 8.33) ambapo watu 21 wamekamtwa.


"Watuhumiwa 21 wamekamatwa kuhusiana na dawa za kulevya zilizokamatwa, baadhi yao wamefikishwa mahakamani na wengine watafikishwa taratibu za kisheria zitakapokamilika" ,amesema Lyimo.


Amezitaja operesheni zilizofanikisha ukamataji wa dawa hizo kuwa ni ilizofanyika jijini Tanga eneo la Mikanjuni tarehe 4 Aprili,2024 ambapo watuhumiwa wawili walikamatwa na gramu 329.412 za heroin, iliyofanyika eneo la Wailes Temeke mtaa wa Jeshini jijini Dar es Salaam tarehe 8 Aprili, 2024 na kufanikisha watuhumiwa wawili kukamatwa na kilogramu 1.49 za skanka, iliyofanyika eneo la Zinga Bagamoyo mkoani Pwani tarehe 10 Aprili, 2024 na kufanikisha kuwakamata watuhumiwa watatu wakiwa na kilogramu 424.84 za dawa ya kulevya aina ya Methamphetamine. Pia mtuhumiwa mwingine mmoja alikamatwa na gramu 158.24 za heroin eneo la Kunduchi jijini Dar es Salaam tarehe 10 Aprili.


"Aidha, tarehe 14 Aprili, 2024 tulifanya operesheni katika eneo la bandari jijini Dar es Salaam na kufanikiwa kukamata kilogramu 4.72 za dawa za kulevya aina ya skanka pamoja na kuwakamata watuhumiwa watatu kuhusika na dawa hizo. Vilevile, tarehe 16 Aprili, 2024 tuliendelea na operesheni jijini Dar es Salaam, katika kata ya Kunduchi na kukamata kilogramu 232.69 za dawa za kulevya aina ya heroin na kilogramu 100.83 za dawa ya kulevya aina ya methamphetamine zilizokuwa zinaingizwa nchini kupitia Bahari ya Hindi. Watuhumiwa waliokamatwa katika tukio hilo ni tisa", amesema Lyimo.

Ameendelea kusema kuwa, mtuhumiwa mmoja alikamatwa tarehe 18 Aprili eneo la bandari jijini Dar es Salaam akiwa na kilogramu 2.12 za skanka.

Pia amefichua mbinu mpya ya ufichaji wa dawa za kulevya inayotumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kusafirisha dawa hizo haramu. Ameeleza kuwa baadhi ya dawa zilizokamatwa zilikuwa zimefichwa kwa ustadi kwenye vifungashio vilivyoandikwa majina ya kahawa na chai ili kukwepa kukamatwa.


Akiangazia tishio la dawa za kulevya linalokua kwa kasi duniani, Kamishna Lyimo ametoa wito kwa jamii kuungana katika kupambana na janga la dawa za kulevya kwani vijana ni kundi linaloathirika zaidi.

"Vijana ni nguvu kazi ya Taifa letu. Kama wakiendelea kuathiriwa na dawa za kulevya, uchumi na usalama wa nchi vitakuwa hatarini. Ni wajibu wa kila mmoja wetu kupambana na janga hili. Tunawaomba wananchi waendelee kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ili kulinda taifa letu dhidi ya janga hili kwa kupiga namba yetu ya bure 119”, amesema Lyimo.

Kamishna Jenerali Lyimo ametoa shukrani kwa wadau wote wanaoshirikiana na DCEA katika vita dhidi ya dawa za kulevya, hasa vyombo vya ulinzi na usalama na kuahidi kuwa DCEA itaendelea kupambana ili kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi salama na isiyo na dawa za kulevya.
Baadhi ya dawa za kulevya zilizokamatwa katika operesheni iliyofanywa na DCEA kuanzia tarehe 4 hadi 18 zikiwa na chapa ya majina ya kahawa na chai kama vile green tea, Dunkin original blend, Krispy Kreme, organic coffee, Taylors of arrogate, after dark ground coffee, French Vannila na asaker prunes.
 
Dawa za kulevya zilizokamatwa Zinga Bagamoyo baada ya kutolewa kwenye viroba.
Picha mbalimbali zinazoonesha jumla ya kilogramu 353.52 za dawa za kulevya zilizokamatwa kata ya Kunduchi jijini Dar es Salaam.
Dawa za kulevya zilizokamatwa Zinga Bagamoyo baada ya kutolewa kwenye viroba.
Magunia ya dawa za kulevya yaliyokamatwa na DCEA yakiwa yaefichwa chooni eneo la zinga Bagamoyo mkoani pwani.
Kilo 1.49 ya dawa za kulevya aina ya skanka zilizokamatwa eneo la Wailes Temeke jijini Dar es Salaam.
Nyumba zilizokamatwa kilo 424.84 za dawa za kulevya aina ya Methamphetamine eneo la zinga Bagamoyo.
Gramu 329.412 za heroin zilizokamatwa Tanga


Share:
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

Popular Posts

Unordered List

Pages

Blog Archive


Copyright © MASWAYETU BLOG | Powered by Blogger